Tuesday, February 28, 2012

Bodaboda 20 watekwa Tabora

E-mail Print PDF
WAENDESHA pikipiki 20 maarufu bodaboda, wametekwa mkoani Tabora, mwaka jana katika matukio ya uhalifu yaliyotokea maeneo tofauti mkoani humo.
Kamamnda wa Polisi mkoani Tabora, Anthony Rutta, alisema katika kipindi hicho, dereva mmoja wa pikipiki alitekwa na kuuawa na watu wasiojulikana baada ya kumkodi.

Alisema katika utekaji huo, polisi walifanikiwa kukamata pikipiki 15, wakati pikipiki 5 hazijapatikana.

Kamanda Rutta, alisema jumla ya watuhumiwa saba walikamatwa na tayari wamefikishwa mahakamani kujibu mashitaka yanayowakabili.

Ili kuondokana na utekaji huo, Kamanda Rutta alisema pamoja na polisi kutoa elimu, pia amewataka waendesha pikipiki wasikubali kukodiwa na mtu wanayemtilia mashaka.

Wakati huo huo, mwendesha pikipiki aliyetambulika kwa jina la Kennedy Lameck amejeruhiwa kwa kukatwa mdomo na mtu aliyetaka kumpora pikipiki .

Kamanda Rutta, alisema tukio hilo lilitokea juzi saa 2 usiku, baada ya mwendesha pikipiki huyo na kukodiwa na mtu asiyemfahamu kumpeleka eneo la Mihogoni.

Alisema baada ya kumshtukia, Lameck alipiga simu kuwafahamisha wenzake, ndipo ghafla mtu huyo alimkata mdomo kwa kisu na kufanikiwa kukimbia.

Kutokana na hali hiyo, Kamanda Rutta aliwataka madereva wa pikipiki kuwa na tahadhari, hasa wanapotakiwa kuwabeba abiria nyakati za usiku.

No comments:

Post a Comment