Tuesday, February 7, 2012

Bunge: Tunamtambua Kafulila, Hamad Rashid


NAIBU Spika wa Bunge, Job Ndugai, amesema Bunge bado linawatambua David Kafulila na Hamad Rashid Mohamed kama wabunge hadi mahakama itakapoamua vinginevyo. Kauli ya Ndugai inakuja baada ya chama cha NCCR-Mageuzi kulalamika kwamba kimedhalilishwa na Bunge baada ya kumteua Kafulila kukiwakilisha chama hicho katika msiba wa Regia Mtema wakati alikwishavuliwa uanachama.

Tangu avuliwe unachama Desemba 17, mwaka jana kisha kukimbilia mahakamani kupinga uamuzi huo, Kafulila amekuwa akiumiza vichwa viongozi wakuu wa chama hicho kutokana na kuendelea na majukumu yake kama kawaida huku akijipambanua kuwa bado ni mwanachama halali wa NCCR-Mageuzi.

Akizungumzia kwa kifupi kuhusu suala hilo, Ndugai alisema NCCR- Mageuzi na Chama cha Wananchi (CUF), wanatakiwa kuwa na subira mpaka kesi walizofungua wabunge wa vyama hivyo zitakapomalizika.
Pia, Ndugai alisema Hamad ambaye Januari 4, mwaka huu alivuliwa uanachama na chama hicho na Kafulila, Bunge bado linawatambua kama wabunge.

“NCCR na CUF wawe na subira ili mahakama itende kazi yake,” alisema Ndugai.Alisema tangu wabunge hao wafungue kesi mahakamani kupinga uamuzi uliochukuliwa na vyama vyao, Bunge linawatambua kuwa bado ni wabunge mpaka hapo mahakama itakapoamua vinginevyo.

Juzi, Kafulila alizidi kuwaumiza vichwa viongozi hao wa NCCR-Mageuzi baada ya Ofisi ya Bunge kumtangaza mbele ya Mwenyekiti James Mbatia kwamba ni mmoja wa wawakilishi wa Bunge wanaokwenda Ifakara katika mazishi ya marehemu Mtema, hatua ambayo jana ilipingwa vikali na chama hicho kupitia kwa Kaimu Katibu Mkuu, George Leonard.

Leonard alisema kitendo hicho cha Bunge ni cha kukidharau chama kwa uamuzi wake wa kumfukuza.Alisema licha ya ofisi za Bunge kufanya kazi yake kwa mujibu wa sheria, kitendo cha kumtangaza Kafulila ilikuwa ni kukidhalilisha na kukifedhehesha chama mbele ya wananchi waliofika maeneo hayo.

"Bunge limekidhalilisha na kufedhehesha chama na wabunge wetu, maana kilichofanyika pale katika viwanja vya Karimjee ni aibu kwa chama,” alisema Leonard na kuongeza:

“Sisi tulimwambia Machali kuwa mwakilishi katika msiba huo, lakini cha ajabu Bunge likamtangaza Kafulia kuwa mwakilishi wa chama wakati wakijua alikwishafukuzwa.”

No comments:

Post a Comment